Allaah سبحانه وتعالى Ametuchagulia Dini ya Kiislamu, Dini ya haki na Hatokubali dini yoyote nyingine. Anasema:
((وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الإِسْلاَمِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ))
((Na anayetafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasirika)) [Al-'Imraan:85]
Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametuambia kuwa kutakua na makundi katika ummah wake ambao watawafuata maadui wa Allaah سبحانه وتعالى katika desturi na mila zao:
((ستتبعون سنن من كان قبلكم شبراً بشبر وذراعاً بذراع حتى لو دخلوا جحر ضب لدخلتموه)) قالوا: أتراهم اليهود والنصارى؟ قال: ((فمن إذن؟)) البخاري ومسلم
((Mtafuata nyendo za wale waliokuja kabla yenu hatua kwa hatua mpaka itafika hadi wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia)) Wakasema (Maswahaba): Ee Mtume! Je, unamaanisha Mayahudi na Manaswara? Akasema: ((Hivyo nani basi mwengine?)) Al-Bukhariy na Muslim
Maneno hayo aliyoyasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakika yamethibiti kwa sababu imedhihirika Waislamu kuigizia mila, desturi na tabia za makafiri na kuzisherehekea kama mfano siku hii inayoitwa 'Valentine day' (Siku ya Wapendanao).
Na baya zaidi na la kusikitisha sana ni kwamba sherehe hizi zinaenezwa katika njia mbali mbali za mawasiliano kama kutumiana kadi, barua pepe (e-mail), salamu katika simu za mkono. Hakika fitna hii humfanya Muislamu aharibu 'Aqiydah (Iymaan) yake kwa kudhani kuwa anafanya jambo la kawaida na hali ni jambo lisilo katika sheria ya dini yetu bali ni shirki kubwa na upotofu wa kufuata wanayoamini makafiri.
Historia Ya Sherehe Ya Siku Ya Valentine
Sherehe hii ya wapendanao ni sherehe ya wapagani wa Kirumi wakati dini yao ya upagani ilikuwa ni dini iliyotapakaa kwa Warumi karne zaidi ya kumi na saba zilizopita. Na fikra zao ilikuwa ni kuelezea hisia ya 'mapenzi ya kiroho'
Kulikuwa na visasili (uongo) zilizohusishwa na sherehe hii ya upagani ya Warumi ambao umeendelea kutoka warithi wa Kikiristo. Miongoni mwa uongo huo ni kuamini kwao Warumi kuwa Romulus, aliyevumbua Rome, alinyonyeshwa siku moja na mbwa mwitu mwanamke, hivyo akampa nguvu na hikma.
Warumi walikuwa wakisherehekea tukio hili katikati ya Februari kila mwaka kwa kufanya sherehe kubwa. Na mojawapo ya tambiko katika sherehe hii ni kuchinja mbwa au mbuzi. Vijana wawili wenye nguvu hujipaka damu ya mbwa au ya mbuzi katika miili yao, kisha huiosha damu hiyo kwa maziwa. Baada ya hapo, watu hufanya gwaride wakiwa vijana hawa wawilii wako mbele wakiongoza gwaride iliyokuwa ikitembea barabarani. Vijana hao wawili walikuwa wakichukua vipande vya ngozi ambavyo waliwapigia watu wanaowavuka. Wanawake wa kirumi walikuwa wakipokea mapigo hayo wakiamini kuwa yatawahifadhi na kutibu utasa.